Home » 2018 » February » 3 » SAFARI 7 ZA AJABU ZA SINDUBAD (Part 3)
18:45
SAFARI 7 ZA AJABU ZA SINDUBAD (Part 3)

SINBAD BAHARIA NA SAFARI ZAKE SABA

SEHEMU YA TATU

SAFARI YA PILI

Kutoka sehemu ya Pili:

Sindubad alipomaliza kuelezea mkasa uliomkuta katika safari yake ya kwanza, watu wote walistaajabu sana kusikia maajabu yale yaliyomkuta, sasa Sindubad anaendelea kuelezea mkasa na maajabu yaliyomkuta katika safari yake ya pili: endelea............

Niliwahadithia jana kwamba, baada ya kupata matatizo makubwa katika safari yangu ya kwanza, nikaazimia kwamba sitosafiri tena na nitabaki katika mji wangu wa Bagdad. Lakini kadiri nilipoendelea kuishi muda mfupi tu, nikachoshwa na maisha ya kukaa tu bila ya kazi yoyote na pia nikachoshwa na maisha ya uvivu. Hivyo nikaamua kusafiri tena, basi nikanunua bidhaa nyingi za kutosha kwaajili ya biashara.

Basi tukaondoka kama ilivyo kawaida pamoja na rafiki zangu katika meli kutoka Bagdad mpaka Basra, tukapita kisiwa hadi kisiwa mji hadi mji huku tukikutana na matajiri wengi tukiuza na kununua bidhaa mpaka tukafika katika kisiwa kikubwa chenye mandhari nzuri sana, chenye miti mingi yenye matunda na mito ya maji baridi.

Basi tukashuka humo, na hatukukuta mtu yeyote katika kisiwa hicho. Tukala matunda ya miti hiyo na tukanywa maji ya mito yake mizuri. Kisha wenzangu wakaanza kuzunguka katika kisiwa hicho wakitazama mambo mbali mbali humo, ila mimi nilibaki peke yangu katika kivuli cha mti mkubwa.

Basi ukanipitia usingizi nikalala, na wala sikujua kwa muda gani nimelala. Hata si muda mrefu, ikanijia fadhaa na hofu, nilikuwa niko mbali na rafiki zangu na wala sikusikia wala kuhisi ishara yao yoyote ile eneo lile.

Hapo sasa nikajua tu kwamba meli yetu imeshaondoka bila ya wenzangu kujua kwamba wameniacha huku, basi nikakimbia mpaka kando ya bahari, nilikuwa kama mwendawazimu kwani ilikuwa tayari imenijia hali ya wasiwasi na huzuni. Nikaiona meli yetu ikiwa mbali sana na inaendelea kutoweka katika upeo wa macho yangu taratibu mpaka ikapotea yote kabisa.

Nikabaki nikiwa na huzuni na hofu kutokana na kusahauliwa kule, nikabaki katika hali ile muda mrefu kidogo. Nikabaki nikijilaumu kuvunja ile azma yangu ya kubaki katika mji wangu bila ya kusafiri. Lakini lawama muda huo zilikuwa hazisaidii kitu.

Basi nikawa nahangaika kuzunguka katika kisiwa kile kutafuta watu lakini sikubahatika kuona mtu hata mmoja. Nikapanda juu ya mti mrefu, huku nikitupa macho katika pembe zote za bahari lakini sikuona chochote isipokuwa maji ya bahari na mbingu.

Nikarejesha macho yangu upande wa kisiwani, nikaona kwa mbali dude kubwa refu jeupe lenye umbo la duara lenye kung’aa kutokana na mwanga wa jua. Nikateremka kutoka kwenye mti na kukimbia kuelekea kwenye dude hilo kwa nguvu zangu zote mpaka nikafika na nikaona dude lile ni refu sana. Nikaligusa kwa mkono wangu nikaona ni lenye umbo la kutereza kama kioo kiasi ambacho si rahisi kwa kiumbe yeyote kulipandia juu. Nikalizunguka pande zote sikuona mlango wa la dirisha. Nilipojaribu kupima mzunguko wake nikapata ni hatua hamsini.

Wakati nipo kwenye hali ya kushangaa dude lile, mara nikaona dunia imeingia giza la ghafla na mwanga wa jua ulipotea kabisa nikawa kwenye giza, nikaangalia juu nikaona ndege mkubwa sana. Palepale nikakumbuka mazungumzo ya wenzangu tuliokuwa tukisafiri pamoja wakizungumzia juu ya ndege aina ya Rukhi na sifa zake zinafanana na huyo ndege nimuonaye sasa.

Vilevile nikagundua kwamba dude lile jeupe lilikuwa ni yai lake. Basi kabla hajatua vizuri nikakaa chini ya lile yai. Akafika chini na kulikumbatia yai kwa mbawa zake na mimi nikalala juu yake. Nikaangalia kucha zake na miguu yake nikaona ni kama mfano wa shina la mti na mizizi yake.

Basi nikavua kilemba changu na kujifunga nacho kwenye mmoja wa miguu yake kwa utaratibu kabisa ili asishituke. Lengo langu aruke na mimi siku inayofatia sehemu nyingine kabisa mbali na kisiwa kile kitupu kisichokuwa na watu.

Basi lengo langu likatimia kwani ilipofika alfajiri tu, ndege yule akaanza kuruka. Akapaa juu kabisa angani mpaka ardhi ikapotea machoni mwangu. Akapaa na mimi kwa muda fulani hivi kisha akatua chini ardhini kwa nguvu mpaka nikazimia. Nikazinduka muda mfupi tu na kumuoona ndege Rukhi amesimama kwenye ardhi. Basi nikajifungua kutoka kwenye ule mguu wake na nilifurahi kuepukana na kile kisiwa chenye kutisha.

Lakini furaha yangu haikudumu kwani nilimuona ndege Rukhi akimeza joka kubwa sana na kupaa angani mpaka akapotea machoni mwangu. Nikaangalia pembezoni mwangu kwakweli nilijuta kukiacha kisiwa kile na kuja kwenye sehemu ile ambayo haiwezi kumuacha mtu yeyote salama. Hakika ndege yule alinileta sehemu mbaya zaidi. Ni bonde kubwa sana tena lenye kina kirefu sana lililozungukwa na milima iliyopanda juu sana kile upande. Hakuna hata sehemu ambayo unaweza ukashikilia na kupanda juu. Basi nikasema na nafsi yangu kwamba, hakika mimi nimeisha sasa ni kifo tu, kila nikiepukana na msiba nakutana na msiba mkubwa zaidi ya wa kwanza.

Na nikaangalia katika bonde lile nilipo, nikaona kuna mawe mengi ya almasi, nikafurahi sana.  Lakini furaha yangu haikudumu kwani pembezoni mwa bonde lile kulikuwa na majoka makubwa sana yenye uwezo wa kumeza hata tembo. Lakini kwa bahati nzuri majoka yale mchana huwa yanajificha kwenye mapango yao kwa kumuogopa ndege Rukhi. Kwasababu ndege Rukhi ndiye adui yao mkubwa sana anayewameza kila siku akitua katika bonde lile. Lakini giza la usiku linapoanza kuingia, majoka yote huanza kutoka katika mapango yao.

Basi nilizunguka katika bonde lile mchana kutwa. Usiku ulipoanza kuingia nikaona sehemu ndogo yenye upenyo nikaingia na kujiziba na jiwe kubwa ili kuepukana na shari ya majoka yale. Nilikula matunda ambayo niliyabeba kutoka katika kile kisiwa cha kwanza.

Nilijaribu kulala lakini sikuweza kupata usingizi kwani nilikuwa nikisikia sauti za majoka yakifokafoka na mengine yakipita karibu na pango nililojificha. Basi sauti zao zilinitia khofu sana, nilibaki katika hali ile usiku kucha.

Basi ilipoingia asubuhi, sauti za majoka zikaisha, nikajua kwamba sasa asubuhi imefika na majoka yote yameingia katika mapango yao. Basi nikamshukuru sana Mwenyezimungu na nikatoka katika pango na kuanza kutembea tembea kwenye bonde lile huku nikifikiria mwisho wa hali ile utakuwa vipi. Kila sehemu ya bonde lile ni mawe ya almasi tupu zenye thamani, lakini nikaona yote hayo kwangu hayakuwa na thamani kuliko ningeona chakula na kinywaji nikaokoa maisha yangu.

Basi nikaona jiwe kubwa kidogo karibu yangu nikakaa na kupumzika kutokana na uchovu mpaka ukanipitia usingizi nikalala palepale. Nilishituliwa na kishindo kidogo, nilipotizama nikaona pande kubwa la nyama lililoanguka pembeni yangu kutoka juu ya bonde lile.

Basi nikakumbuka habari ya wafanya biashara katika bonde la almasi na njia zao wanazozitumia kupata almasi katika bonde lile. Ni kwamba wao huchinja kondoo na kumchuna, kisha huenda mpaka juu ya bonde lile na kutupa zile nyama chini ya bonde, nyama zile zikianguka chini hugandana na mawe ya almasi. Baada ya muda mfupi huja tai wengi na kushuka mpaka chini ya bonde kwaajili ya kuchukua nyama zile mpaka juu nje ya bonde.

Tai wale wakishapanda na nyama zile juu ya bonde, wafanyabiashara huwatishia kwa kuwafukuza na kuwapiga, basi tai huziachia nyama zile na kukimbia. Hapo wafanyabiashara huziokota nyama zile na kutoa almasi zilizoganda kwenye nyama kisha huziacha nyama kwaajili ya wale tai.

Basi nilijua kwamba huenda habari hii ya hawa wafanyabiashara ni hadithi tu za watu zisizo na ukweli. Lakini kwa hali hii najionea kwa macho yangu kwamba maneno yale ni kweli kabisa.

Basi nikaona sasa hii ndio njia ya kuokoka. Nikaokota kiasi cha almasi chenye kunitosheleza kisha nikalala chini kwa mgongo wangu na juu yangu nikashikilia pande moja la nyama kwa nguvu zangu zote. Basi akaja tai mmoja mkubwa sana na kulichukua lile pande la nyama nililolishikilia na kupanda nalo juu ya bonde mpaka akafika juu kabisa nje ya bonde lile na kuliachia pande lile la nyama.

Basi wafanya biashara wakakimbia kumtisha yule tai mkubwa naye akaogopa na kukimbia na kuliacha lile pande la nyama pale juu, kisha nikainuka. Mmoja wa wafanyabiashara wale aliponiona akaogopa na alipoangalia katika lile pande la nyama hakuona almasi yoyote iliyoganda, basi akalia na kujipiga usoni kwa kuona bahati yake ilivyo mbaya kwa kukosa almasi na akizingatia kwamba alihangaika sana kuchinja na mpaka kufika pale.

Basi nikamsogelea na kumtuliza kisha nikampa almasi nyingi sana katika zile nilizokusanya chini ya bonde. Basi huzuni yake ikabadilika na kuwa furaha kubwa sana, kisha akaniuliza juu ya kufika kwangu pale nami nikamuhadithia yote yaliyonikuta. Akashituka sana na wale waliokuwa naye pia walishituka kusikia kisa change kile.

Kisha nikasafiri nao mpaka kwenye mji wangu. Hakika niliona njiani mambo mengi ya ajabu sana, tulisafiri mchana na usiku mpaka tukafika Bagdad. Nilikuwa na almasi nyingi sana zenye thamani kubwa sana zisizo na kipimo.

Nilipoingia tu mjini kwangu, walinipokea jamaa zangu kwa furaha sana kutokana na kurudi kwangu kwa salama. Nikawasaidia masikini na fukara na nikaweka azma ya kutosafiri tena na kubaki mjini kwangu Bagdad katika umri wangu wote.

Sindubad alipomaliza kusimulia, akaamuru Hindubad apewe dinar mia moja, akamshukuru sana na kumuombea dua. Kisha wote wakatawanyika kwaajili ya kurudi kesho kusikiliza yaliyomkuta Sindubad katika safari yake ya tatu.

 

Je kuna nini kwenye safari ya tatu? Usikose kuisoma sehemu inayofuata.

Category: Stories & Entertainment | Views: 1352 | Added by: badshah | Rating: 1.5/2
Total comments: 2
2 rose  
0 Spam
I'm enjoying to Read this story....

1 Suleiman Hemed  
0 Spam
smile smile smile smile

Name *:
Email *:
Code *: