Home » 2017 » December » 16 » Alibaba na wezi 40 Part 13
19:13
Alibaba na wezi 40 Part 13

SEHEMU YA KUMI NA TATU

JIHADHARI SANA ALIBABA!!!

 

Kutoka sehemu ya kumi na mbili:

Marjane agundua siri ya kiongozi wa wezi, kwa ujanja wake afanikiwa kuwauwa wezi wote thelathini na tisa bila ya kumjulisha yeyote ndani ya nyumba na bila hata ya vurugu yoyote kutokea ndani ya nyumba. Kiongozi wezi agundua kwamba wenzake wote wameshauliwa bila ya yeye kufahamu, sasa atambua kwamba hayuko salama ndani ya ile nyumba na kwa siri aamua kutoroka kwa kuruka ukuta wa nyuma ya nyumba ile. Alibaba asubuhi sana anatoka nje kuelekea bafuni na kukuta mitungi bado ipo na mategemeo yake ni kwamba mgeni ataondoka mapema sana. Lakini Alibaba aliamini kwamba huenda mgeni bado amelala kutokana na uchovu wa safari .............

Endelea sehemu ya Kumi na tatu.

Alibaba alipotoka bafuni bado aliiona mitungi ile arobaini pale uwani na muda ulikuwa umeenda kidogo, akilinganisha kauli ya mgeni wake kwamba angeondoka asubuhi sana kuelekea kwenye safari yake ya kuuza mafuta.

“Marjane!” Alibaba aliita, “Mbona muuza mafuta bado hajaondoka?”

Marjane akatoka jikoni. “Nitakuelezea kila kitu bosi wangu.”Marjane alisema.  “Lakini kwanza hebu angalia ndani ya mitungi hiyo.”

Alibaba alichanganyikiwa kidogo kusikia hivyo. Akasogea na kufunua mfuniko wa mtungi mmoja.

“Kuna mtu humu!” alisema kwa mshtuko. “Tena amekufa!!”

Aliangalia katika kila mtungi. “Watu thelathini na tisa waliokufa ndani ya mitungi na mtungi mmoja una mafuta kidogo! Kumetokea nini Marjane?”

“Kuna mtu anajaribu kukuua, bosi,” Marjane alijibu. “Kuna siku niliona alama nyeupe ya chaki kwenye mlango wa mbele wa nyumba yetu. Nikajua huenda kuna mtu ameweka alama hiyo kwa siri na pia nikajua tu kwamba kuna kitu kibaya kinaendelea, hivyo nikaamua kuweka alama kama ile katika kila mlango wa mbele wa nyumba zote za mtaani hapa.”

“Siku nyingine nikaona alama ndogo nyekundu kwenye fremu ya dirisha. Basi nikafanya vilevile katika nyumba za mtaani.”

“Sasa jana,” Marjane aliendelea kuelezea. “Muuza mafuta alikuja na punda wake ishirini na mitungi ishirini ya mafuta kama unavyojua bosi. Usiku wa jana ulipokuwa umelala, niliamua kuandaa chakula cha leo mchana kabisa, hivyo nilihitaji mafuta zaidi kwaajili ya taa ya chemni, hivyo nilienda kule uwani kwenye mitungi ili nichukue mafuta kidogo tu kutoka katika ile mitungi. Sasa nilipoenda kwenye mtungi wa kwanza ili nichukue mafuta. Nikaanza kufunua mfuniko wa mtungi, mara nikasikia sauti ikitoka ndani ya mtungi ikiuliza, “Vipi muda tayari tutoke kwaajili ya mapambano?”

Marjane alinyamaza kidogo akimuangalia Alibaba. Kisha akaendelea kuelezea. “basi sikuwa na cha kufanya. Ila nikaijibu ile sauti iliyouliza nikasema ‘Bado – ila muda mfupi tu nitawajulisha!’ nikaenda kwenye mtungi wa pili, hali ikawa ni ileile, na wa tatu pia—na wa nne na wa tano mpaka mitungi thelathini na tisa hali ilikuwa ni ileile na mimi nikajibu vilevile kwa sauti nzito kidogo inayofanana na ya muuza mafuta. Isipokuwa mtungi wa arobaini ndio uliokuwa na mafuta ndani. Nikajua tu kwamba kwa hali ile bosi wangu uko hatarini hivyo nikachemsha mafuta mengi sana yaliyotoka kwenye ule mtungi wa arobaini na nikayamimina katika kila mtungi. Nafikiri bosi sasa unaelewa stori nzima.”

Alibaba alishtuka sana kusikia hivyo. Alisimama kwa muda kidogo kimya na kufikiri kwa haraka sana.

“Sina adui yoyote hapa mjini,” Alijisemea moyoni. “Lakini kuna hazina niliziiba kutoka kwenye lile pango la ajabu msituni na wezi walimuua kaka yangu Kassim. Sasa nafikiri wanajaribu kutaka kuniua na mimi. Lakini hawatafanikiwa!”

Kisha akasema, “Umefanya vizuri sana Marjane. Umeokoa maisha yangu. Nafikiri huyu muuza mafuta ni kiongozi wa wale wezi waliomuua Kassim, nafikir wanataka kuniua na mimi kwasababu nilichukua dhahabu zao. Lakini yuko wapi sasa huyo muuza mafuta?”

“Sijui, bosi,” Marjane alijibu. “Hata chumbani hayupo, nafikiri alikimbia usiku.”

Ulipoungia usiku, wakati mkewe amelala, Alibaba alimuita kijana wake Khalid na wakachukua masepetu mawili na kuchimba shimo kubwa sana chini ya bustani yao. Katika shimo hilo, waliwazika wezi wote thelathini na tisa pamoja na mitungi yote arobaini. Lakini walizificha panga zao na mikuki ndani ya nyumba kwasababu walijua kwamba huenda kuna siku watazihitaji.

Asubuhi, Alibaba aliwaswaga punda wote ishirini sokoni na kuwauza wote.

“Nimewazika wezi wote thelathini na tisa na mitungi, na nimeficha silaha zao,” Alibaba alimwambia Marjane.  “Pia nimeuza punda wote ishirini. Lakini bado kuna tatizo moja. Kiongozi wa wezi bado yuko huru! Huenda akajaribu kuniuwa tena!”

Wakati ule, kiongozi wa wezi alikuwa amejificha msituni ndani ya lile pango. Akiwa ameshika tama kwa huzuni.

Baada ya kukimbia kutoka kwa Alibaba, alielekea moja kwa moja mpaka msituni. Alikuwa na hasira na aibu pia kwasababu mpango wake ulishindikana.

Bado kulikuwa na hazina nyingi sana katika pango. Lakini hili halikumfurahisha. Alikuwa mpweke sana. Kwasababu watu wake wote waliuliwa kule kwa Alibaba. Hakuwa na mtu wa kuongea nae – hakuna mtu wa kumuheshimu – wala hakuna mtu wa kumwambia maneno mazuri. Alibaki tu kufikiria kwamba, ni lazima amuue Alibaba!!!!!

Hivyo basi kiongozi wa wezi alikaa pangoni kwa wiki kadhaa akitengeneza mpango mwingine.

“Lazima niwe mwerevu sana,” alijisema mwenyewe. “kuna mtu katika ile nyumba ni mwerevu pia. Na ndio maana sasa niko hapa peke yangu. Sasa lazima nifanye urafiki na Alibaba. Kwa njia hiyo nitaweza kuingia ndani ya nyumba ya Alibaba. Nitamuua hali ya kuwa hakutarajia. Huenda nikaamua wakati tunapata chakula cha jioni.”

Kiongozi wa wezi akaamua kujifunika uso kiasi ambacho hakuna mtu ndani ya nyumba ya Alibaba angeweza kumtambua. Alivaa ndefu za bandia na akanyoa nywele zake zote na kuwa na kipara.

Kisha, kiongozi wa wezi akaamua kutumia dhahabu zake kununua duka kubwa pale mjini. Akaanza kulijaza duka lake vitambaa mbalimbali vya hariri alivyokuwa amevihifadhi pangoni. Watu wengi sana walikuja dukani kwake na kununua vitambaa vile vizuri. Na muda mfupi tu kiongozi yule wa wezi akawa maarufu sana kama mfanya biashara mkubwa wa kuuza vitambaa vya hariri. Pia alijipatia jina na kujiita: Khoja Hussein.

Alipokuwa akiuza vitambaa kwa wateja wake, alikuwa pia akiwasikiliza wakizungumzia kuhusu watu tofauti wa pale mjini. Vilevile alifanya urafiki na wafanya biashara wakubwa wa pale mjini. Alitaka kwa hali yoyote ile kufahamu kwa undani kuhusu Alibaba na watu anaoishi nao katika ile nyumba. Siku moja alikwenda kumtembelea mfanya biashara mdogo wa mazulia aitwae Khalid. Duka la Khalid lilikuwa mtaa mmoja na duka lake.

“Habari za asubuhi,” Khoja alimsalimia kijana yule. Khalid alikuwa akikunjua zulia refu jekundu akimuonesha mteja wake pale dukani.

“Jina kangu ni Khoja Hussein na ni mgeni hapa mjini. Naona una mazulia mazuri sana!”

“Ahsante,” kijana alijibu. “Baba yangu mkubwa Kassim alianzisha biashara hii, lakini alikuja kuuawa katika mazingira ya kutisha sana.”

“Heh! Na ilikuwaje ikawa hivyo sasa?” Khoja aliuliza.

“Aliuliwa na wezi msituni!” Khalid alielezea.

Khoja alisogea mbele kidogo na kuonesha mshangao usoni.

“Kifo cha kutisha!” alisema. “umesema alikuwa ni baba yako mkubwa – ina maana ni kaka wa baba yako?”

“ndio,” Khalid alijibu.

“Na je baba yako yuko hai leo?” Khoja aliuliza.

“Oh , ndio,” Khalid alijibu. “Ninaishi naye sasa pamoja na mama yangu na mama yangu mkubwa ambaye ni mke wa marehemu baba yangu mkubwa.”

“Na baba yako anaitwa nani?” Khoja Hussein aliuliza.

“Jina lake ni Alibaba!” Khalid alijibu.

Siku inayofuata, Khoja Hussein alirudi pale dukani kwa Khalid.

“Nilifurahia mazungumzo yetu jana,” alimwambia muuza mazulia. “nafikiri tunaweza tukawa marafiki wazuri sana. Unaweza ukaja kwangu kupata chakula cha jioni leo.”

Hivyo wawili hao walipata chakula cha jioni pamoja na baada ya hapo wakawa ni wenye kuonana kila siku. Wakati mwingine Khalid alikwenda kwenye duka la Khoja Hussein na wakati mwingine Khoja Hussein alikwenda kwenye duka la Khalid na kuzungumzia mambo mbalimbali yahusuyo vitambaa vya hariri na mazulia na kuhusu wateja wao.

Siku moja, wakati Khoja Hussein amemtembelea rafiki yake Khalid katika duka lake la mazulia, kulikuwa na mtu mwingine pale dukani. Alikuwa akizungumzia kuhusu kununua zulia jipya kwaajili ya nyumbani kwao. Khoja Hussein akamuangali yule mtu kwa umakini kabisa. Alikuwa na uhakika kabisa kwamba huyo mtu ni yule adui yake, Alibaba!!! Kisha Khoja Hussein akaondoka pale dukani haraka sana. Hakutaka Alibaba amuone.

Siku iliyofuata, Khalid alimtembelea Khoja Hussein dukani kwake.

“Yule mtu aliyekuja kukuona jana,” alisema Khoja Hussein.  “Anafanana sana na rafiki yangu. Alikuwa nani yule?”

“Yule ni baba yangu, Alibaba,” Khalid alijibu.

Baada ya hapo wote wakaenda kupata chakula cha jioni katika hoteli kubwa iliyoko maeneo ya pale mjini kama kawaida yao.

Jioni moja, wakati Khalid na Khoja Hussein wakiwa katika matembezi yao mjini pale, Khalid akasimama nje ya nyumba moja kubwa yenye mlango wa bluu.

“Hii ni nyumba ya baba yangu,” Khalid alimwambia rafiki yake. “Hapa ndipo tunapoishi. Nimemuelezea baba yote kuhusu wewe – duka lako, vitambaa unavyouza vizuri na upole wako na ukarimu wako kwangu. Anataka kuonana na wewe.”

“Ni mkarimu sana, Khalid,” Khoja alijibu. “Lakini huenda baba yako akawa na kazi nyingi sana jioni hii.”

“Hawezi kuwa na kazi nyingi kiasi cha kushindwa kumkaribisha rafiki yangu kipenzi,” Khalid alijibu.

Kisha akafungua mlango na kumkaribisha Khoja Hussein ndani ya nyumba yao.

Endelea sehemu ya kumi na nne ya hadithi hii…………….

 

Category: Stories & Entertainment | Views: 641 | Added by: badshah | Rating: 4.0/1
Total comments: 0
Name *:
Email *:
Code *: