Home » 2017 » October » 8 » Alibaba na wezi 40 Part 3
00:13
Alibaba na wezi 40 Part 3

SEHEMU YA TATU

Kutoka sehemu ya pili:

Baada ya mke wa alibaba kurudisha mizani kwa mke wa kassim na kujulikana kilichotendeka huko kuwa sio nyama iliyopimwa bali ni dhahabu. “Nilijua tu hawa walikuwa na siri!, wamepata wapi hii dhahabu?” Alisema mke wa Kassim……… Endelea sehemu ya tatu:
 

Mumewe aliporudi, alimuonesha ile sarafu ya dhahabu iliyokuwa imeganda chini ya ile mizani. “Angalia mume wangu!” alisema mke wa kassim, “Mke wa Alibaba alikuja kuniazima mizani ili akapimie nyama, mimi sikumuamini nikapaka asali chini ya mizani, na angalia sasa aliporudisha nikaona hii sarafu ya dhahabu imenata huku kwenye asali bila ya wao kujua, na ndio imenisaidia kujua walichokuwa wanakipima”.

Kassim alipoangalia kwenye ile mizani na kuona ile sarafu ya dhahabu alishtuka sana. “Mimi ni tajiri!” alisema Kassim “lakini Alibaba atakuwa tajiri kunishinda mimi, lazima niende nikamuulize amepata wapi dhahabu zote hizi, inaelekea ni nyingi sana mpaka anaamua kuzipima kwenye mizani!!”. Hapana mume wangu” Alijibu mkewe,”Usiende sasa hivi ni usiku sana, wewe lala kwanza upumzike kisha kesho asubuhi ndio uende, lazima watuambie kila kitu, hawawezi kuficha siri hii”. “sawa mke wangu nimekuelewa” alisema Kassim, “nitaenda huko asubuhi”.

Mwisho wa Sura ya Kwanza

SURA YA PILI:

KUINGIA MTEGONI

Je Kassim alikuwa na furaha juu ya mafanikio ya ndugu yake? Hapana! Hakuwa na furaha bali ni wivu. Kassim hakulala usiku ule na alikuwa hafikirii chochote isipokuwa Alibaba na Dhahabu tu usiku kucha.

“Sio haki kabisa!” alijisemea Kassim. “Nimefanya kazi kwa bidii miaka yote hii kuhakikisha kwamba napata hela za kutosha, na mpaka sasa mimi ni tajiri, lakini Alibaba alikuwa kazi yake ni kukata kuni na kuuza mjini na kupata hela kidogo sana. Amepata wapi dhahabu hizi? Nani atakuwa amempa? Lazima nijue tu na mimi nipate za kwangu”.

Jua lilipochomoza tu, Kassim aliamka huku amekunja sura. “Sio vizuri kabisa!” Alisema. “nitaenda kuzungumza naye nijue kila kitu, ndugu hawawezi kufichiana siri kiasi hiki.”

“Vizuri sana!” alijibu mke wake. “Tena nenda na ile mizani ukamuoneshe  sarafu ya dhahabu iliyonata kule chini, hii itasaidia kumfanya atambue kwamba tumeshagundua siri zao.”

“Hilo ni wazo zuri!” alisema Kassim. “kwahiyo nenda jikoni kailete haraka niwahi huko.”

Basi Kassim kwa mwendo wa kasi na wa tamaa kubwa sana kama mtu anayewahi sehemu fulani muhimu sana, alivuka mtaa wa pili mpaka kwa kijijumba kidogo cha ndugu yake Alibaba, kisha akapiga hodi.

Alibaba akaja kumfungulia na ikawa ni ajabu sana kumuona kaka yake pale.

“Habari yako, Kassim”. Alisalimia Alibaba. “Tafadhali ingia ndani na uniambie mbona ni asubuhi sana upo hapa kwangu?”

“Najua siri yako, Alibaba!” alijibu Kassim. “Unasema kwamba wewe ni masikini mkata kuni, lakini kumbe una dhahabu nyingi sana mpaka unazipima! Umezipata wapi ndugu yangu?”

Alibaba akajifanya kama hajui kitu na kushangaa. “Dhahabu?” alisema Alibaba. “una maana gani? Mimi sina dhahabu, mimi ni masikini kama unavyonijua, mimi naenda msituni kila siku kukata kuni, tajiri hafanyi hivyo, ningekuwa tajiri ningekuwa na maisha mazuri, ningekaa katika jumba kubwa la kifahari, ningekuwa nakunywa maziwa na asali”

Baada ya Alibaba kumaliza kusema hayo, Kassim alinyanyua ile mizani usawa wa uso wa alibaba na kutabasamu. “Mkeo aliazima hii jana” Kassim alimwambia Alibaba. “Alisema kwamba alitaka akapimie nyama. Mke wangu alishangaa sana kusikia hivyo, alijua kuwa nyinyi ni masikini sana hamuwezi kununua nyama, hivyo alipata hamu ya kujua kama kweli ni nyama basi ni ya aina gani, hivyo akapaka asali chini yake ili kipande kidogo kikiganda ajue ni nyama ya aina gani mlionunua, lakini kumbe sio nyama ni dhahabu kama unavyoona nimekuja kukuonesha imeganda kwenye asali hapa chini. Unaona sasa, tunajua siri zenu, kumbe mlikuwa hampimi nyama bali ni dhahabu. Nataka uniambie kila kitu kuhusu hizi dhahabu.”

Alibaba hakuwa na la kujitetea na hata mkewe pia alibaki hana la kusema kutokana na kwamba kila kitu kimejulikana na ushahidi wa hilo umeonekana.

Alibaba aliamua kumueleza ukweli wote kuhusu dhahabu zile, alimpa stori yote kuhusu wale watu 40 wenye farasi, na maajabu ya pango lile jinsi linavyofunguka kwa kutamka yale maneno ya ajabu na kufunga kwa kutamka yale maneno ya ajabu, pia alimueleza kuhusu vitu vilivyopo ndani ya pango lile.

“Hiyo ndio stori nzima ya dhahabu hizi” alisema Alibaba.

“Sasa na mimi pia nataka hizo dhahabu!” Alisema Kassim kwa tamaa. “nielekeze hilo pango lilipo na mimi niende”

“Nitakuelekeza hilo pango lilipo”, alijibu Alibaba. “lakini kumbuka kwamba kachukue dhahabu kidogo tu zilizobaki niachie ni za kwangu”.

Kassim akakubali. Alibaba akamuelekeza maeneo lilipo hilo pango. Kassim akaondoka mpaka kwakwe kwaajili ya maandalizi ya kwenda huko pangoni siku inayofuata.

***** MWISHO WA SEHEMU YA TATU *****

 

Usikose sehemu ya nne ya hadithi hii.

Category: Stories & Entertainment | Views: 696 | Added by: Admin | Rating: 2.0/1
Total comments: 5
5 hafsa  
0 Spam
Stori nzuri sana.tuendrleze part 4

3 kipe  
0 Spam
Hadirahaaa Fanya hadi part 5 tongue  good

4 Admin  
0
Usijali zinakuja muda si mrefu

1 briliant  
0 Spam
Wawooooo tongue

2 Admin  
0

Name *:
Email *:
Code *: