Home » 2017 » October » 9 » Alibaba na wezi 40 Part 4
21:15
Alibaba na wezi 40 Part 4

SEHEMU YA NNE

Kutoka sehemu ya tatu:

Kassim alipoenda kwa ndugu yake na kumshawishi amwambie mahala alipozitoa dhahabu zile, Alibaba hatimaye alimweleza ukweli wote. Sasa Kassim amerudi kwake kujiandaa na safari ya msituni mahala ambapo pango linapatikana.

ENDELEA SEHEMU YA NNE

Asubuhi ilipofika kabla ya jua kuchomoza, Kassim alimuaga mke wake na kuelekea msituni. Alienda huko na punda kumi wenye masanduku makubwa sana mgongoni, Kassim alikuwa ni mwenye tamaa, hakutaka dhahabu kidogo kama walivyokubaliana na ndugu yake, alitaka achukue zote.

Alifuata maelekezo yote ya Alibaba mpaka akafika kwenye jiwe kubwa la rangi ya kijivu, hiyo ndiyo ilikuwa alama. Aliwasimamisha punda wake nje ya pango.

“Sasa ngoja niseme yale maneno” alijisemea Kassim. “Fungukaaaa sesmiii”. Mara pango likafunguka. Kassim alikuwa na shauku na furaha alipoona hivyo, akakimbilia haraka sana ndani ya pango. Alipokuwa ndani ya pango akasema, “Fungaaaaa sesmiiii!!” na hapo pango likajifunga.

Kulikuwa na hazina nyingi sana! Kassim alishusha na kupandisha pumzi kwa nguvu kwa jinsi alivyokuwa haamini macho yake. Kulikuwa na mapande ya dhahabu, sarafu zinazong’aa sana na vito vyenye thamani na rangi nzuri nzuri.

Kila kitu kilikua kinawakawaka kwa mng’aro uliosababishwa na mwanga kutoka nje kwa kupitia matundu madogo ya pango lile. Kassim akachukua bangili  zilizotengenezwa kwa madini ya rubi, na akachukua pia mkanda ambao umepambwa na almasi zenye kung’aa sana. Vilevile akachukua mkufu uliotengenezwa kwa madini ya safaya. Rangi yake ni kama rangi ya mbingu. Uzuri gani wa vitu vile ulikuwa siku hiyo!

Kassim alibeba kila kitu anachotaka mle pangoni mafungu kwa mafungu na kuzipeleka karibu na mlango wa pango ili iwe rahisi kuzipeleka kwa wale punda wake kumi wakati atakapolifungua pango lile. Ilikuwa ni kazi ngumu sana. Pia hakutosheka akarudi tena kuchukua sarafu za dhahabu, alibeba mafurushi mengi makubwa makubwa ya sarafu za dhahabu mpaka kwenye mlango wa pango lile. Kazi yake kubwa ilikuwa ni kukusanya kila kitu na kusogeza kwenye mlango wa pango.

“Sasa ni wakati wa kuondoka”, alijisemea Kassim. “sitaki kukaa hapa muda mrefu mwishowe wale wezi wanikute humu watakaporudi! Nimeshapata mali nyingi sana ya kutosha kujaza masanduku yote kumi yaliyobebwa na punda wangu. Nitarudi kesho na siku inayofuata na inayofuata hivyohivyo mpaka mali yote hii niimalize, lakini kwa leo inatosha wacha tu nirudi nyumbani”

Kwahiyo basi, Kassim akaanza kusema yale maneno ya siri yakufungulia pango lile ili atoke nje. “Fungukaaaaa ……….!!!” Lakini alisahau neno linalofuata! Alijaribu tena, “Fungukaaaa…..uummh!!!” , loh! masikini Kassim kasahau kabisa neno linalofuata. Akajaribu kwa mara nyingine tena. “Fungukaaaa…eeee ssssiiisss!!!, hapana sio hivyo, ah nimeshasahau neno lile! Mlango uliendelea kuwa umefunga kwa kuwa neno lile Kassim hakuweza kulikumbuka ambalo ndio la kufungulia lango lile. Kassim akaanza kutetemeka kwa hofu. Akaanza kuvuja jasho. Alikuwa na hazina nyingi pale kashazikusanya lakini hazitasaidia kitu chochote endapo mlango utashindwa kufunguka.

“Muda wote nilikuwa nafikiria mali tu na kusahau neno la siri!”, alilia Kassim. Alijilaumu sana. “ Sasa nimekamatika leo” alisema Kassim. Alitupa begi la dhahabu alillokuwa amelibeba na kulipiga teke kama mpira wa miguu. “nilifikiri nitakuwa tajiri sana, kumbe ni marehemu mtarajiwa” Alijiwazia Kassim.

Mara Kassim akasikia sauti ambayo ilibadilisha damu yake kuwa barafu. Alisikia sauti za kwato za farasi zikija kwa vishindo kutoka mbali kidogo. Walikuwa ni farasi wapatao arobaini (40) na walikuwa wameshakaribia kufika kwenye mlango wa pango lile.

“Fanyeni haraka! Tuziweke hizi hazina ili tuondoke haraka tukatafute tajiri mwingine wa kumuibia!” Kiongozi wao alisema. Na huku wenzake wakiwa wakicheka. Walikuwa wanakuja kuweka mali pangoni ambazo wametoka kuziiba.

Lakini walipokaribia kufika katika jiwe kubwa la pango, kiongozi wao akaona kitu ambacho kilimkasirisha sana. Kulikuwa na punda kumi waliokuwa wamesimama nje ya pango lile wakiwa na masanduku makubwa juu ya migongo yao.

“Kuna mtu anajaribu kutuibia mali zetu!!”, kiongozi wao alisema. “Lazima tumkomeshe mara moja!!”.  Wale wezi walipiga makelele ya hasira huku wakipiga makofi, punda wote kumi walishikwa na hofu na kukimbilia msituni. Kwa taratibu  kabisa wezi wote walishikilia panga zao kali huku wakikaribia lango la pango lile.

Fungukaaaaa sesmiii!!!”, alisema Kiongozi wao. Lango kubwa la jiwe likaanza kufunguka. Ghafla Kassim alitoka mbio nje kulekea kwa kiongozi wa wale wezi huku akipiga makelele na kumkamata na kuanza kupigana. Alijitahidi sana kupigana ili aweze kuokoa maisha yake, lakini mmoja kati ya wale wezi alimchoma panga tumboni na hatimaye Kassim akaanguka na kufa palepale.

Wezi wale arobaini walimuacha Kassim chini na kuingia pangoni, “angalia hii mifuko ya dhahabu hapa mlangoni!!” alisema mmoja wa wale wezi, “huyu alikuwa amepanga kuzichukua hizi zote na kuzipeleka kwa wale punda wake kumi!”.

“Alikuwa peke yake huyu?” Aliuliza kiongozi wao. “kwasababu baadhi ya dhahabu zipo hapa mlangoni na zingine hazipo kabisa humu pangoni!, huenda ni zaidi ya mtu mmoja alikuwepo humu pangoni wakiiba hazina zetu! kwahiyo watu wawili wamegundua neon letu la siri la kufunguli apango hili!!”

“Sasa sijui tufanye nini” alisema mmoja wa wale wezi.

“Tumemuua mmoja!” Alisema kiongozi wao. “ Na huyu mwingine tutamtisha kwa njia moja ama nyingine, hatathubutu tena kutuibia chochote hapa!!”. Alinyanyua upanga wake juu hewani huku akitoka nje ya pango.

“Chukua hii maiti ya huyu jamaa mkaining’inize juu ndani ya pango!!” Alisema kiongozi wao. “Mwili wake utakuwa ni onyo kwa yeyote atayekuja humu ndani!”. Ilikuwa inatisha sana.

Hivyo basi, wezi wakachukua kamba na kuuning’iniza mwili wa Kassim juu ndani ya pango na kisha wakatoka kulekea kwenye farasi wao tayari kwa safari ya kwenda mjini tena kuiba.

“Pango letu limeshakaribia kujaa dhahabu” Alisema kiongozi wao. “Na muda si mrefu tutapata nyingine zaidi!”. Baada ya kusema hayo wakaondoka zao wote.

Nini kitaendelea? usikose sehemu ya tano ya hadithi hii yenye kusisimua.

 

Category: Stories & Entertainment | Views: 750 | Added by: Admin | Rating: 2.0/1
Total comments: 3
3 akidas  
0 Spam
Fantastic

2 don  
0 Spam
Nzuri sanaaa

1 kipe  
0 Spam
Habitat sir part5 usiikose tongue tongue

Name *:
Email *:
Code *: