Home » 2017 » November » 1 » Alibaba na wezi 40 Part 8
19:32
Alibaba na wezi 40 Part 8

SEHEMU YA NANE

Kutoka sehemu ya saba:

Baada ya yule mwizi kuhangaika mchana kutwa na hatimaye kupumzika katika kijiduka cha fundi  mshona nguo, katika kujisifu utaalamu wake, fundi anajikuta anatoboa siri na kumfanya yule mwizi kuwa makini sana kutaka kujua habari hii.

ENDELEA SEHEMU YA NANE

Yule mwizi akamsogelea fundi kwa karibu zaidi na kutaka kujizuia na ule mshangao aliouonesha aliposikia kuhusu maiti. “Tafadhali hebu niambie huyo maiti alikufa vipi?” mwizi alimuuliza fundi.

“siwezi kukwambia zaidi kuhusu maiti huyo” fundi alijibu. “Ni siri na nimemuahidi msichana wa watu kuwa nitaitunza siri hii.”

Mwizi akachukua sarafu moja ya dhahabu kutoka katika lile vazi lake refu na kumuonesha fundi nguo. “Unaitwa nani mzee wangu?” Mwizi aliuliza. “Mustafa” fundi nguo akajibu.

“Vizuri, Mustafa, sitaki kujua jina la aliyefariki” mwizi alisema huku akitabasamu, “sitaki kujua kitu chochote kuhusu yeye, wewe nipeleke tu nyumbani kwake na nitakulipa vizuri sana.”

Mustafa alifikiri kwa muda mfupi kidogo. Kisha akachukua ile sarafu ya dhahabu.

“Nitajaribu” Mustafa alisema, “lakini yule msichana alinichukua hali ya kuwa amenifunga macho na kitambaa hivyo sitaweza kupajua.”

“Twende sasa hivi,” alisema mwizi. “Utajifunga macho na kitambaa vilevile kama ulivyofanya mwanzo. Vilevile utalazimika kurudi nyumbani katika hali hiyohiyo ili usipajue nyumbani hapo ukaonekana ni mvunjaji wa ahadi. Hata kama utakua huoni wakati tunaenda lakini utatumia harufu za maua na sauti za wanyama kuweza kutambua njia. Jitahidi sana na nitakulipa vizuri sana.”

Alipomaliza kusema hayo akachukua sarafu nyingine ya dhahabu na kumuongezea Mustafa. “Nitajaribu,” alisema Mustafa huku akitabasamu.

Mustafa akamalizia kushona viatu vya mwizi huyo kisha akafunga kibanda chake. Mwizi akachkua kitambaa kirefu cha njano na kumfunga Mustafa kuzunguka kichwa ili azibe macho yake.

“Sawa kabisa!, sasa jifanye kama ulivyofanya mwanzo” alisema mwizi, “Mimi niwe kama yule msichana wa kazi, sasa jaribu kutafuta sauti njiani na harufu harufu ambazo ulikuwa ukizisikia wakati unapelekwa na yule msichana mara ya kwanza.”

Waote wawili wakaanza safari. Mwizi alimshika mkono Mustafa ili aweze kumuongoza vizuri njiani

Baada ya muda mfupi, Mustafa akasimama na kusikilizia harufu. “Nyama ya kuku!” alisema. “Kuna mtu anapika nyama ya kuku kwaajili ya chakula cha jioni. Inanukia vizuri sana, hii nyumba wanapenda sana nyama ya kuku jioni, sasa nina uhakika hii ni njia yenyewe.”

Dakika chache baadaye, Mustafa akasema, “nasikia sauti za punda maeneo fulani kushotoni kwetu, hiyo ndio njia inatakiwa tuifuate.”

Dakika chache baadaye, alisimama na kusema,”hiyo sauti ninayoisikia ni ya mtoto analia, hako katoto kila siku jioni lazima kalie tu, labda hakataki kwenda kulala mapema, nafikiri hiyo ndio njia yenyewe huko na nafikiri tunakaribia kufika mahala husika sasa.”

Waliendelea na safari kidogo tena, Mustafa akasimama na kuvuta harufu na kusema, “nakumbuka hii harufu ni ya maua mazuri sana ambayo nayapenda sana, hii harufu niliwahi kuisikia sehemu moja tu ambayo ndio ile nyumba tunayoitafuta. Nafikiri hapa ndipo mahala tunapohitaji rafiki yangu. Hii ndio nyumba yenyewe, hii ndio nyumba ambayo nilikuja kushona suti ya yule marehemu tuliyekuwa tukimzungumzia.”

Harufu ile ya maua mazuri ilikuwa ikitokea kwenye dirisha zuri la nyumba ya Kassim. Mustafa ameweza kumuongoza mwizi mpaka pale kwenye ile nyumba.

“Una uhakika kwamba hii ndio nyumba yenyewe?” mwizi aliuliza.

“Ndio kabisaaaa nina uhakika kabisa hapa ndipo penyewe.” Mustafa alijibu. “Ila tu siufahamu huu mtaa hivyo hata nyumba yenyewe siwezi kuijua ni ya nani.”

“Hiyo haijalishi. Umenielekeza vya kutosha” alisema mwizi. “umekuwa na msaada mkubwa sana kwangu. Sasa chukua hii sarafu nyingine tena ya dhahabu na nitakuongoza urudi kwenye kibanda chako cha kushonea nguo.

Mwizi akatoa kipande cha chaki kutoka mfukoni kwake na kuweka alama kwenye mlango wa nje wa nyumba ile.

“Hapa sasa nimeshamaliza kazi” alijisemea mwizi. “Nimeweka alama hii mlangoni ili iwe rahisi kwangu kuja. Kwa maana nyumba zote mtaa huu zinafanana, hivyo haitakuwa rahisi kukumbuka. Hii alama ya chaki mlangoni ndio itanikumbusha nitakapokuja kwa mara ya pili. Hapo tutaweza kuvamia na mapanga yetu na kumuua huyu mwizi wa pili wa hazina zetu kule pangoni”

Mwizi akamchukua Mustafa na kumrudisha kibandani kwake kisha akaanza safari ya kurudi msituni kuungana na wezi wenzake. “kiongozi wangu atafurahi sana kwa kazi yangu!” alijisemea huku akicheka. Alipokuwa njiani juu ya farasi wake akawa anawaza jinsi wenzake watakavyokuwa na furaha kupata habari njema ile.

Asubuhi iliyofuata, yule msichana wa kazi Marjane alianza kuandaa chai ya asubuhi kwaajili ya Alibaba na familia nzima. Alichukua birika yenye kahawa na kuandaa machungwa pamoja na sahani na vikombe. Lakini akagundua kwamba hakuna mkate jikoni.

“Itabidi tu nikanunue mkate haraka” alijisemea huku akichukua mfuko na kuelekea madukani hapo mjini. Alipokuwa akirudi, wakati anakaribia mlangoni, akaona alama nyeupe asiyoielewa, akasogea kwa karibu zaidi na kuitazama, ni alama ya chaki imechorwa mlangoni.

“Hii alama haikuwako hapa jana!” alijisemea. “Nani atakuwa ameweka alama hii hapa mlangoni? Na itakuwa ina maana gani hii alama?” Marjane alisimama pale muda kidogo huku akitafakari na kukuna kidevi chake kama mtu anayetafuta ufumbuzi wa jambo fulani.

“Simjui nani aliyeweka hii alama hapa.” Alisema. “sijui pia aliyeweka alikuwa ana maana gani- lakini nafikiri hii alama itakuwa si alama nzuri kabisa. Najua nini cha kufanya.” Akaingia ndani na kuchukua kipande cha chaki. Kisha akatoka nje na kuzunguka mtaa mzima na kuweka alama kama ile mlangoni katika kila mlango wa nyumba zote za mtaani pale.

“Hii lazima itamchanganya huyu anayetaka kufanya ubaya katika nyumba yetu.” Alijisemea huku akitabasamu. Kisha akarudi ndani kumalizia kuandaa chai. Hakumwambia yeyote kuhusu ile alama ya chaki.

Endelea sehemu ya tisa ya hadithi hii…………….

 

Category: Stories & Entertainment | Views: 651 | Added by: Admin | Rating: 3.5/2
Total comments: 3
2 don  
0 Spam
It is the best even if it is long, sir if there is another long story please can you give smile smile smile

3 badshah  
0
Yeah there are so many stories and very interesting, dont worry

1 barbie  
0 Spam
It's good but it's too long

Name *:
Email *:
Code *: