Home » 2018 » March » 8 » SAFARI 7 ZA AJABU ZA SINDUBAD (Part 4)
22:11
SAFARI 7 ZA AJABU ZA SINDUBAD (Part 4)

SINBAD BAHARIA NA SAFARI ZAKE SABA

SEHEMU YA NNE

SAFARI YA TATU

Kutoka sehemu ya tatu:

 

Sindubad alipomaliza kuelezea mkasa uliomkuta katika safari yake ya pili, watu wote walistaajabu sana kusikia maajabu yale yaliyomkuta, sasa Sindubad anaendelea kuelezea mkasa na maajabu yaliyomkuta katika safari yake ya tatu: endelea............

Baada ya kurudi kutoka katika safari yangu ya pili, niliazimia kutosafiri tena na nikaamua kubaki katika mji wangu maisha yangu yote yaliyobaki. Lakini nafsi yangu haikuridhika kukaa maisha ya uvivu na starehe.

Basi nikanunua bidhaa nyingi sana na nikasafiri kutoka Bagdad mpaka Basra tukiwa mimi na baadhi ya matajiri wengine katika meli kubwa iliyokuwa ikitupitisha maeneo mbali mbali ya miji  tukinunua na kuuza bidhaa na tukapata faida nyingi sana. Wakati tupo njiani katika bahari, ghafla ukapiga upepo mkali sana ulisukuma mawimbi makubwa yaliyoyumbisha meli yetu, ulitutisha sana tukajua sasa ni kuangamia tu na hakuna njia yoyote.

Hali ile iliendelea mpaka tukapotea njia. Tukaishi katika hali ya kutangatanga baharini kwenye meli yetu siku nzima, mpaka kikatokezea mbele yetu kisiwa kikubwa sana. Tulipofika, nahodha wa meli yetu akashuka katika ardhi ya kisiwa kile na akaonekana kushikwa na huzuni kubwa sana na kusema,  “hakika tumeshaangamia na matumaini ya kukoka kwetu yamekwishapotea.”

Tukamuuliza sababu ya kusema vile naye akajibu, “hakika kisiwa hiki na vinginevyo vilivyo karibu yake, huishi watu wafupi sana wajulikanao kama mbilikimo wasiostaarabika, na wao katika mapango yao humu ni wengi sana na wala hakuna hata mmoja wetu mwenye uwezo wa kushindana nao.”

Wala hakumaliza kusema maneno hayo, na ghafla wakatuzunguka watu hao wafupi wasiostaarabika, walikuwa kila mmoja wao urefu wake hauzidi nyayo mbili za mguu, na miili yao ilifunikwa na manyoya mekundu na walizungumza lugha ambazo hatukuzifahamu.

Basi walizunguka meli yetu na kutuamuru tushuke na hatukuweza kupambana nao kwa jinsi walivyokuwa wengi sana, hivyo tukajisalimisha kwao. Kisha wakatushusha katika meli yetu na kuipeleka mahali tusipopajua na wakatuacha peke yetu tukiwa hatujui tufanye nini.

Tukaamua kuondoka tukizunguka katika kisiwa kile hali ya kuwa hatuna matumaini ya kuokoka kutokana na hali iliyotukuta. Wakati tupo katika mizunguko ya hapa na pale, mara kwa mbali tukaona jumba kubwa sana, basi tukalikaribia jumba lile na tulipofika tukaona ni kama kasri au ngome kubwa sana iliyopanda juu sana hewani. Basi sote tukaingia ndani kupitia mlango wake mkubwa wa mbele uliokuwa wazi. Kisha tukaingia mpaka uwani kwakwe tukakuta mafungu ya mifupa ya watu. Hali ile ilishtua sana mioyo yetu. Na wala hakuna hata mmoja wetu aliyetamka neno hata moja kutokana na shida ya vitisho vile. Basi tukabaki katika hofu ile mchana kutwa mpaka jua likazama, na mara tukasikia mlio wa mlango ukifungulia na ukafungwa. Tukaliona jitu kubwa sana refu lenye kimo kinachofanana na mnazi, lenye uso mweusi sana na usoni lina jicho moja tu lenye kutoa mwanga kama wa moto mwekundu,  na lenye meno mawili marefu na makali kama ya nyoka.

Tulipoliona vile, tulizidi kuwa na uwoga na miili yetu ilitetemeka sana kwa hofu na tulikuwa kama wafu. Basi akatutazama kwa kuogopa na mara kanisogolea na kunikamata katika kiganja chake, nilikuwa kama ndege mdogo katika mkono wake, basi akaniona kuwa ni mwembamba sana na mwili wangu hauna nyama, basi akaniachia, akamkamata mwengine wetu vilevile akamuona ni mwembamba na hana nyama naye pia akamuachia.

Basi alipogeuza jicho lake kwa nahodha wetu, akashangaa kumuona mnene na mwili umejaa nyama, basi akamnyakua kwa mkono wake kisha akaenda sehemu kidogo na kutoa chuma kirefu chembamba chenye ncha kali kama cha kutungia mishikaki, basi akamchoma nacho nahodha wetu kuanzia utosini mpaka miguuni, kisha akakoka moto na akambanika kama mshikaki. Basi haikupita muda mrefu nyama yake iliiva naye akala nyama yote ya nahodha wetu na kutupa mifupa yake ardhini.

Kisha akalala na tukasikia akikoroma kwa nguvu. Kulipopambazuka, jitu lile likatoka nje ya jumba lile na kutuacha ndani, nasi tukatoka tukizunguka zunguka huku na huko katika kisiwa, tulitamani bora tungekufa tu ndani ya maji kuliko kuwa katika hali ile ya vitisho vikubwa sana na vifo vyenye mateso na maumivu makali.

Tuliendelea kuzunguka katika kisiwa mchana kutwa tukitafuta sehemu ambayo tutajistiri na kujificha lakini hatukuweza kupata sehemu yoyote. Tukarudi katika jumba lile tukiwa tumejawa na hofu, na lile jitu kama kawaida likaja na kumchukua mmoja wetu na kumchoma na kumla kama alivyomfanya nahodha wetu jana, na likalala mpaka asubuhi, kisha likaondoka bila ya sisi kujua. Na sisi pia tukatoka kuzunguka zunguka katika kisiwa, basi baadhi ya rafiki zangu wakashauriana kwamba tujitose tu baharini kuliko kuteseka na kifo kile cha kuchomwa na kuliwa nyama. Lakini baadhi wakashauriana kwamba ni bora tujipange tuliuwe jitu lile.

Pia na mimi nikawashauri kwamba tuandae gogo kubwa la mti na tulitengeneze kama mtumbwi ambalo endapo tutashindwa kuliua jitu lile basi tukimbie na tujitose baharini katika mtumbwi ule, basi wakafurahi rafiki zangu kwa ushauri ule. Tukaanza kazi yakuandaa gogo lile na kutengeneza mtumbwi mpaka ukakamilika, kisha tukaufunga pembezoni mwa bahari.

Na tukarudi katika jumba lile, basi kama kawaida yake likaja jitu lile na kumla mmoja wetu tena kama lilivyowala wale wenzetu waliotangulia, kisha likalala na kukoroma kwa nguvu kama kawaida yake. Kisha tukachukua vyuma vile anavyotumia kuwabanika wenzetu na tukaviweka viwili katika moto aliokuwa ameukoka mpaka vikawa vyekundu kabisa. Kisha tukamchoma navyo kwa nguvu kabisa katika lile jicho lake hali ya kuwa amelala, akashituka sana na kupiga ukelele mkubwa sana kutokana na shida ya maumivu makali, na akasimama akitapatapa kama mwendawazimu akitutafuta kwa kupapasa baada ya jicho lake kupofuka, lakini hakuweza kumshika hata mmoja wetu.

Basi akaenda mpaka mlangoni na kufungua mlango na kutoka nje. Tulifurahi sana na tukajua sasa tumeshaingiwa na amani na tumeshaokoka kutokana na jitu lile. Lakini furaha yetu haikudumu kwani walikuja kundi kubwa la majitu kama lile baada ya muda mfupi tu, wakiwa hawana tofauti kabisa na lile jitu la kwanza na wenye roho mbaya vilevile kama lile jitu. Basi tukawakimbia tukielekea katika mtumbwi tulioutengeneza.

Walipotuona ndani ya bahari, wakajitosa na wao baharini wakiwa na mawe makubwa sana na kuturushia, basi wakawauwa marafiki zangu. Na wala hawakuokoka pamoja nami isipokuwa wenzangu wawili tu.

Na baada ya kuokoka kutokana na shari ya majitu yale, tuliogelea kwenye mawimbi ya bahari mchana wetu na usiku wetu, mpaka kulipopambazuka, mawimbi yalitupeleka mpaka pembezoni mwa kisiwa kikubwa. Tulifurahi sana na tulikula matunda ya kisiwa hicho mazuri na tukanywa maji. Kisha tukakaa kandokando ya bahari tukiwa na furaha ya kuokoka na majitu ya kisiwa kile.

Na ilipofika usiku, tulilala juu ya mti mrefu na tukashituka na kupatwa hofu pale tulipoona chatu  mkubwa sana akiwa amemkamata mmoja wa rafiki zangu, na tukasikia mifupa yake ikivunjika na kisha akammeza. Tukaona sasa hali bado sio nzuri na tukasema, “hakuna hila wala nguvu isipokuwa kwa mwenyezimungu mkuu. Kila tukiepukana na shari, huja shari nyingine”.

Basi ilipofika asubuhi, tukanywa na kula mpaka ikafika tena usiku, tukapanda juu ya mti mwingine tena na nikalala juu kabisa, na rafiki yangu akalala karibu yangu. Na baada ya muda mfupi tu, akaja tena chatu na kumkamata rafiki yangu kama alivyomkamata yule wa jana!

Nilikesha usiku kucha nikiwa na hofu, na sasa niko peke yangu mpaka kulipokucha, nikaona ni bora tu nijitose baharini nife. Lakini bado nilikuwa na hamu ya kuishi hivyo nikabadilisha uamuzi huo. Na ilipofika usiku, nikachukua mapande ya magogo na mbao mbao zilizokuwa karibu yangu nikajifunga nazo mwili mzima na kuzikaza kabisa.

Basi kama kawaida ya yule chatu akaja tena ili aimalizie na mimi, akanichukua kwa mdomo wake na kujaribu kutaka kunimeza lakini hali ilikuwa ngumu kwakwe kutokana na ugumu wa mbao nilizojifunga nazo mwili mzima, alijaribu kila hila usiku kucha bila ya mafanikio mpaka kukapambazuka, naye alipona jua linaanza kuchomoza akatoweka.

Nikamshukuru sana mwenyezimungu na nikajifungua kutoka katika mbao zile nikiwa salama kabisa na sikudhurika chochote katika mwili wangu.

Basi nikakaa kando ya bahari nikitafakari jinsi gani naweza kuokoka kutokana na madhila niliyoyapata, na mara kwa mbali nikaona meli kubwa. Nikaaza kupiga kelele za kuiita huku nikiashiria kwa mkono wangu na huku nikipunga juu kwa kutumia kilemba changu mpaka baadhi ya watu wa meli ile waliniona.

Basi wakaja karibu na kisiwa kile kisha wakashuka kutoka kwenye meli, nikawasilimia nao wakaniitikia salamu yangu. Nilifurahi sana kukutana nao furaha kubwa sana. Basi wakanichukua pamoja nao, wakaniuliza juu ya mimi kuwa pale, nikawahadithia kisa chote kilichonikuta. Wakashituka sana kusikia vile, nao wakanikarimu vizuri sana.

Na tulipokaribia kufika katika mji mmoja mkubwa, nahodha wa meli akaniambia kwamba, “kuna bidhaa ninazo za mtu mmoja aitwaye Sindubad, tulikuwa naye lakini kwa bahati mbaya tulimsahau katika kisiwa kimoja katika safari zetu.”

Basi yule nahodha aliponiangalia vizuri ndipo nikamtambua, nikamwambia kwamba mimi ndiye Sindubad. Hakuweza kuniamini kwa mara moja hivyo, basi walikuwepo baadhi ya wafanyabiashara wakinizunguka pale, na kulikuwa na mmoja wao ambaye nilishikilia nyama yake ili kuokoka na bonde la majoka makubwa wakati wakiwa wanatafuta almasi  katika safari iliyopita, naye aliponiangalia tu akanikumbuka na kawahadithia yaliyotokea pamoja naye katika hiyo safari iliyopita. Basi nahodha wa meli ile aliposikia hivyo akajaribu kuniangalia vizuri tena ndipo aliponikumbuka na kuamini maneno yangu, basi alinikumbatia kwa furaha kubwa kabisa.

Basi tuliendelea na safari yetu kutoka mji mmoja hadi mwingine, kisiwa kimoja hadi kingine huku tukiendelea na biashara yetu, mpaka tukafika mji wa Basra, kisha nikasafiri kutoka Basra mpaka mjini kwangu Bagdad nikiwa na mali nyingi sana hazielezeki.

Basi wakanikaribisha ndugu zangu na jamaa zangu na marafiki wakinifurahia na kunipongeza kwa kurudi kwangu salama. Hakika walifurahi sana furaha isiyo na kipimo.

Basi alipomaliza kuhadithia kisa cha safari hii ya tatu. Akaamuru Hindubad apewe dinari mia moja. Basi Hindubad akamshukuru sana na kumuombea dua kisha wote wakatawanyika.

Siku iliyofuata wote wakakusanyika tena kwaajili ya kusikiliza kisa cha safari ya nne.

Usikose kufuatalia kisa hiki.......................

Category: Stories & Entertainment | Views: 1122 | Added by: badshah | Rating: 4.7/3
Total comments: 0
Name *:
Email *:
Code *: