Home » 2017 » October » 18 » Alibaba na wezi 40 Part 6
20:02
Alibaba na wezi 40 Part 6

SEHEMU YA SITA

MAZISHI YA KASSIM

Kutoka sehemu ya tano:

Alibaba aliamua kwenda msituni ili kumtafuta kaka yake, lakini kwa bahati mbaya akakuta kaka yake alishauliwa na wezi wale 40 na maiti ya kaka yake huyo kuning’inizwa juu ya pango ndani. Kwa huzuni kubwa sana Alibaba aliichukua maiti ile pamoja na dhahabu kidogo kutoka pangoni na kuifikisha nyumbani kwakwe kwanza kabla ya kuipeleka kwa mke wa marehemu kaka yake. Baada ya kufika nyumbani Alibaba akaampa mkewe dhahabu zile afukie wakati yeye anaipeleka maiti ya kaka yake kwa mkewe.

ENDELEA SEHEMU YA SITA

Alibaba alipofika mlangoni kwa nyumba ya Kassim akagonga mlango, mfanyakazi wa Kassim aitwae Marjane akaja kumfungulia. Alibaba alimtazama Marjane kwa hali ya kuwa na matumaini fulani kwasababu alikuwa ni msichana muaminifu sana na alimuamini sana.

Marjane alipouona mwili wa bosi wake, ghafla akanyanyua mikono mpaka mdomoni na akatumbua macho kwa mshtuko na hofu.

“Kassim alikwenda msituni kwenda kuchukua dhahabu” alisema Alibaba kumwambia Marjane, “na dhahabu zile ni za wezi ambao walimfuma Kassim pangoni na kumuua.”

“ila nina wazo” aliendelea kusema Alibaba, “nitauficha mwili huu kwenye ghala chini, halafu tutasingizia kwamba Kassim anaumwa na ameamua kupumzika chumbani kwake. Halafu baada ya siku tatu tutasema kwamba Kassim amefariki kutokana na ugonjwa. Sasa nenda ukamwambie bosi wako (mke wa Kassim) kuhusu habari hizi mbaya. Ila usimwambie mtu yeyote mwingine kuhusu jambo hili.”

Alibaba akauficha mwili wa Kassim katika ghala kisha akarudi kwenye kijumba chake kidogo.

“Sasa Kassim ameshafariki” Alibaba alimwambia mkewe, “mke wa kassim hatataka kuishi peke yake. Nafikiri bora tuhame hapa twende tukaishi kwake na tuondoke na dhahabu zetu zote. Pia, nyumba ya Kassim ni kubwa kuliko hii yetu. Na Marjane mfanyakazi wake atatusaidia kazi sote pamoja na tutamlipa dhahabu kidogo.”

Hivyo basi, ilipofika jioni, Alibaba, mkewe na mtoto wao aitwae Khalid walihama na vitu vyao vyote mpaka kwenye nyumba ya Kassim. Ilipofika usiku, Alibaba akarudi kule nyumbani kwake kwa zamani na kufukua zile dhahabu kisha kwa siri akazipeleka kwenye makazi yao mapya.

Asubuhi ya siku iliyofuata, Marjane msichana wa kazi akaenda kwenye duka la dawa. Duka lilikuwa limejaa watu wengi wa mjini pale. Marjane kwa makusudi akaongea kwa nguvu ili kuhakikisha kila aliye pale anasikia.

“Nahitaji msaada wako!!” alisema Marjane kwa kulia, “anaumwa sana!!! Naomba nipatie vidonge ili nikampatie aweze kupata nafuu!”

Muuza duka alikuwa akitengeneza dawa, kamuangalia Marjane. “Nani anaumwa - Na nini kinamsumbua zaidi?” Aliuliza muuza dawa.

“Ni bosi wangu, Kassim. Anaumwa sana,” Marjane alijibu huku akitokwa na machozi. “hawezi kula wala kuongea na anapata maumivu makali sana. Unaweza kunipatia vidonge tafadhali?”

Muuza duka akachukua chupa ndogo iliyokuwa na vidonge vyeupe kisha akampatia Marjane. “ hizi zitampa nafuu, mpe vidonge viwili kila baada ya saa mbili.”

“Ahsante sana!” alisema Marjane. Kisha akaenda nyumbani na kusubiri.

Kesho yake asubuhi, alirudi kwa muuza dawa tena. Kwa mara nyingine tena akaongea kwa nguvu ili kila aliye pale dukani asikie anachokisema.

“Bosi wangu Kassim hajapata nafuu hata kidogo!” alisema Marjane kumwambia muuza dawa. “badala yake sasa hali inazidi kuwa mbaya, unaweza kunipatia dawa nyingine  ili aweze kupata nafuu?”

Muuza dawa alitikisa kichwa kwa kusikitikia hali ya Kassim. “Pole sana, kwa kusikia hali ya Kassim kuwa mbaya kiasi hicho” alisema huku akichukua chupa ya dawa na kumpa Marjane. “Mpe hii anywe vijiko viwili itamfanya apate usingizi na maumivu yatapungua.”

“Ahsante sana” alijibu Marjane na kuondoka kwenda nyumbani.

Jioni ya siku inayofuata, jua lilipokuwa linazama, baadhi ya watu walikuwa wakipita katika nyumba ya Kassim, wakasikia kilio kikali sana. Alikuwa ni mke wa Kassim.

“Kassim amefarikiii!!!” alilia mke wa Kassim. “Masikini mume wanguuuu!! Umefarikiii!! Nitafanya nini mimiiiii!!!

Marjane akaenda kwa fundi wa nguo aitwaye Mustafa. “Mustafa!” Marjane alisema huku akimuwekea sarafu ya dhahabu mkononi kwake. “Nimesikia watu wakisema kuwa wewe ni fundi nguo mzuri sana hapa mjini. Nina kazi ngumu sana nataka kukupa. Kumetokea ajali na kuna mtu amefariki kwa ajali hiyo, hivyo basi, nataka umtengenezee suti nzuuuri sana ili tuweze kumzika vizuri. Tutakulipa vizuri sana ila usimwambie mtu yeyote kuhusu hili. Mtu huyo ameuliwa kwa kukatwa na mapanga hivyo hakikisha hakuna mtu atakayeweza kuona alama yeyote ile.”

Mustafa akaangalia ile dhahabu aliyowekewa mkononi. “Nitaifanya usiwe na wasiwasi” alisema. “Lakini nitahitaji dhahabu nyingine zaidi ili niweze kuifanya hii kuwa ni siri.”

“Utapata zaidi dhahabu, usijali” alijibu Marjane. “Lakini lazima uifanye kuwa ni siri. Sitakwambia kuwa mtu mwenyewe ni nani na anaishi wapi. Nitakapokupeleka kwake lazima uvae kitambaa machoni ili usiweze kujua ni wapi.”

“Vizuri sana!” alijibu Mustafa fundi nguo. “Nitafanya kama ulivyosema.”

“Sawa basi, chukua sindano yako na uzi” Marjane alimwambia. “kisha twende huko pamoja sasa.”

Marjane akachukua kilemba change na kumfunga fundi vizuri machoni kuzunguka kichwa chake. “Unaweza kuona chochote?” alimuuliza.

“Sioni chochote” fundi alimjibu.

“Vizuri!! Sasa twende nyumbani sasa hivi” alimwambia.

Marjane alimuongoza Mustafa mpaka nyumbani kwa Kassim na kumpeleka hadi kwenye ghala ambapo ulihifadhiwa mwili wa Kassim. Kisha akamfungua kile kitambaa machoni na kuuona ule mwili.

“Unataka nimtengenezee huyu suti!!? Ni kazi ngumu sana.” Alisema Mustafa. “Nahitaji dhahabu nyingine zaidi!”

“Utapata,” alijibu Marjane na kuweka sarafu mbili nyingine za dhahabu kwenye mkono wa Mustafa. “Lakini unatakiwa uanze kushona sasa hivi kwasababu tunataka kumzika huyu  usiku huu huu.”

Mustafa akachukua sindano na uzi wake na kuanza kushona.

Mustafa alishona kwa muda mrefu sana huku Marjane akimsubiri kwa wasiwasi. Mustafa alipomaliza kushona suti nzuri ya hariri alifungasha vifaa vyake kisha Marjane akamfunga tena machoni kile kitambaa na kumuongoza tena kurudi hadi nyumbani kwake.

Walipofika, Marjane akamfungua kile kitambaa na kukiweka begani kwake. “Sasa unaweza kuendelea na kazi zako zingine.” Alisema Marjane kumwambia Fundi Mustafa, “sahau kila kilichotokea siku ya leo.”

Wakati Marjane akiondoka alipofika mbali kidogo akasimama nyuma ya kibanda cha muuza mafuta na kumuangalia Mustafa.  Alitaka kuhakikisha kwamba Mustafa hamuangalii na kumfuatilia kule anapoenda, lakini Mustafa aliendelea tu na kazi yake ya kushona.

Kisha Marjane akarudi nyumbani kwa Kassim ambapo Alibaba na mkewe na mke wa Kassim walikuwa wakimsubiria.

“Tunaweza kumzika sasa” Marjane alisema.

Alibaba na wake wawili wakaanza kumvisha nguo Kassim na kumpeleka mpaka makaburini. Imamu akasoma dua za kumuombea Kassim na wanawake watatu wale wakaanza kulia kwa huzuni. Alibaba aliangalia chini ardhini na kufuta machozi yaliyokuwa yakimtoka kwa huzuni ya kumpoteza kaka yake.

Baada ya mazishi, mke wa Alibaba akasema, “tunaishi katika nyumba ya Kassim, lakini tutafanya nini kuhusu lile duka lake? Nani atakuwa akiliangalia?”

Alibaba akafikiri kwa muda kidogo. “Nitampatia duka hilo mtoto wetu Khalid,” alisema.

Endelea sehemu ya saba ya hadithi hii…………….

 

Category: Stories & Entertainment | Views: 304 | Added by: badshah | Rating: 3.5/2
Total comments: 4
0 Spam
4 goku  
Nzuri smile smile smile smile smile [color=blue] cry

0 Spam
3 zakwan  
Very very interesting

0 Spam
2 mannor  
Interestng

0 Spam
1 don  
Nzuri zanaaa

Name *:
Email *:
All emoticons
Code *: